Thursday, July 26, 2012

DAU LAZAMA NA KUUA ZANZIBAR

0 comments
SALMA SALIM HASSAN, ZANZIBAR
Dau lililokuwa limebaba abiria na mizigo limepinduka na kuzama katika pwani ya bahari ya Hindi, eneo la Mkoani Kisiwani Pemba.
     Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba, Hassan Nassir alisema Dau hilo limezama majira ya saa 11 alfajiri ya leo, ikitokea bandari bubu eneo la Mkoani kuelekea Kijiji cha Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja.
     Katika tukio hilo mtoto mwenye umri wa miaka mitano amefariki dunia ambaye alikuwa pamoja na mama yake Sharifa Mohammed ambaye ameokolewa akiwa na mtoto wake mwengine mwenye umri wa miaka miwili.
     Watu wengine waliokuwamo kwenye  dau hilo hali zao sio nzuri na wamelazwa katika Hospitali ya Abdallah  Mzee Wilaya ya Mkoani Mkoa Kusini Pemba kwa matibabu.
    Waliolazwa ni pamoja na Salum Suluhu, Juma Siasa Abdallah, Ali Denge na Abdallah Omar Kombo ambaye hali yake ni mbaya. Majeruhi wengine walipatiwa matibabu na kuruhusiwa kurejea nyumbani.
     Kamanda huyo wa Polisi alisema wanamshikilia Nahodha wa Dau hilo Omar Juma Ali(29) mkazi wa Kangani Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini  Pemba na anatarajwia kufikishwa mahakamani wakati wowote baada ya upelelezi kukamilika.
    Wakati tukio hilo likitokea, bado wananchi wamo katika maafa ya kuzama kwa meli ya Mv. Skagit iliyokuwa ikitokea bandari ya Dar es Salaam kwenda Zanzibar . Watu 94 wamepoteza maisha na 146 waliokolewa wakiwa hai.
      Meli ya Mv. Skagit ilizama Julai 18,2012 karibu na Kisiwa cha Chumbe umbali wa maili sita kuelekea Kusini mwa Kisiwa kidogo cha Yasin Zanzibar ikitokea Bandari ya Dar es Salaam ilikoanza safari saa 5:30 asubuhi.
      Meli hiyo inamilikiwa na Kampuni ya Sea Guall Sea Transport Ltd, Kampuni ambayo Meli yake nyengine ya Mv. Fatih ilizama ikiwa Bandarini Malindi Zanzibar na kufariki watu sita mwaka 2009.

0 comments:

Post a Comment

Mdau mtandao huu ni kwa ajili yako, weka maoni yao uelimishane na wenzako, Zingatia kutoleta maoni yanayochafua hali ya Hewa! Sasa Endelea....