Tuesday, July 10, 2012

KAMATI YA BUNGE YA NUU YAMALIZA ZIARA YAKE NEW YORK

0 comments

Na Mwandishi Maalum. New York
Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya  Nje, Ulinzi na Usalama ( NUU) Mhe. Edward Lowassa (Mb), amewaasa Maafisa wa Ubalozi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania katika Umoja wa Mataifa,  kutotetereka wala kuyumba  pale inapowapasa kutoa misimamo kwa maslahi ya  nchi yao.
Ametoa wasia  huo  wakati alipokuwa akitoa majumuisho ya ziara ya kamati yake, ziara ambayo pamoja na mambo  mengine ililenga kujifunza na kujionea hali hali ya mazingira ya utendaji kazi ya maafisa wanaoiwakilisha  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.
 Akimnukuu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Mhe. Lowassa alikuwa na haya ya kusema.
“ Mwalimu aliwahi kutueleza huko nyuma kwamba,  jambo linaloipa heshima kubwa  Tanzania licha ya  umaskini wake ni namna isivyotetereka katika  kukisema na kukitetea kile inachokiamini hata kama kinawaudhi wakubwa. Kwa  hiyo  nami ninapenda kwanza, kuwapongeza kwa utendaji wenu wa kazi, lakini kubwa na la msingi msiogope kutetea misimamo ya nchi yenu licha  ya umaskini wetu” akasema  Mwenyekiti wa Kamati.
Akizungumza kwa niaba ya  wajumbe wa  Kamati hiyo inayowajumuisha Mhe.Beatrice Shelukindo,Mhe. Rachel Masishanga, Mhe. Khalifa Khalifa na Mhe. Vita Kawawa. Mhe. Edward Lowassa, licha wa kuwaasa maafia hao kutolegeza buti zao pale linapokuja suala la kusimamia na kutetea maslahi ya taifa na utaifa. Amewapongeza maafisa hao kwa namna wavyofanya kazi kwa uhodari mkubwa ikiwa ni pamoja na  ushirikiano wa hali ya juu wanaouonyesha miongoni mwao.
  Tukiwa hapa tumejifunza mengi, tumeona mengi, tumefahamu changamoto mnazikabiliana nazo katika utekelezaji wa majukumu yenu ya kila siku. Lakini pia tumefurahishwa na kuridhishwa  sana na mpangilio  wa kazi zenu, ushirikiano  miongoni mwenu, mshikamano na maelewano ambayo mmejijengea, hili ni jambo jema sana na  tunawaomba mliendeleze”. Akasisitiza Mwenyekiti.
Aidha  Mhe Lowassa,  akasema  Kamati yake itakwenda kuzifanya kazi changamoto mbalimbali kwa kushirikiana na wahusika  kwa lengo la kuboresha mazingira ya kazi  ili kuleta ufanisi zaidi na tija.
Katika hatua nyingine   Mwenyekiti amewahimiza maafisa hao umuhimu wa kujiendeleza kitaaluma  na kusisitiza kwamba elimu haina mwisho na hasa katika  dunia ya leo ambayo inachangamoto za kila aina.
Kwa upande wake Kaibu Balozi, Dkt. Justin Seruhere akizungumza kwa niaba ya maafisa wenzie ameishukuru kamati hiyo kwa kuutembelea Ubalozi na kuahidi  kwamba maafisa watazifanyia kazi changamoto zilizoainishwa na wajumbe wa   kamati wakati wa ziara hiyo.
 Wakiwa hapa  New York ujumbe wa Kamati ya Mambo ya  Nje, Ulinzi na Usalama walipata fursa ya kusikiliza taarifa za utendaji kazi  wa kila  Afisa kulingana na majukumu ya Kamati yake, taarifa ya masuala ya utawala na fedha na wakapata pia   fursa ya kuhudhuria mikutano na mijadala iliyokuwa ikiendelea  katika Umoja wa Mataifa, na wakatembelea na kukagua  majengo yanayomilikiwa na serikali na  yale ambayo  yamekodishwa.

0 comments:

Post a Comment

Mdau mtandao huu ni kwa ajili yako, weka maoni yao uelimishane na wenzako, Zingatia kutoleta maoni yanayochafua hali ya Hewa! Sasa Endelea....