Saturday, July 28, 2012

MKATABA WA KUDHIBITI BIASHARA YA SILAHA DUNIANI WAKWAMA

0 comments

NA MWANDISHI MAALUM, NEW YORK
 Matarajio na matumaini ya  kupatikana  Mkataba wa Kisheria wa  Kudhibiti Biashara ya  Silaha Duniani ( ATT) yameishia ukiongoni baada ya nchi wanachama kushindwa kuzikabili tofauti za  kimsimamo na kimaslahi.
Kuanzia  tarehe Mbili hadi 27 mwezi huu wa Julai  ,  wajumbe kutoka mataifa  karibu  yote duniani ikiwamo Palestina na Holly Sea, na  Vyama  Kiraia walikutana  hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa kwa lengo moja kuu na muhimu sana,  mstakabali wa biashara ya silaha duniani.
Pamoja na kujadiliana , wakati mwingine hadi usiku wa manane kuhusu umuhimu na malengo ya kuwa na  Mkataba huo, nchi hizo hazikuweza kukubaliana kuwa na mkataba ambao ungesimamia ununuzi na matumizi ya  silaha za aina mbalimbali  zikiwamo pia risasi.
 Kutofikiwa kwa  Mkataba huo licha ya kutolewa kwa rasimu ambayo ilijitahidi kukidhi matarajio na maslahi ya kila nchi kumetokana na kutokukubaliana kwa vipengele vichache ambavyo baadhi ya nchi zilitaka viingizwe.
Vipengele ambayo  vilishindikana kupatiwa ufumbuzi hadi siku ya mwisho ya majadiliano ni pamoja na,  Baadhi ya Nchi zinazouza na kuzalisha silaha kutokuwa tayari kuingiza kwenye mkataba huo risasi na  mabomu, huku nchi nyingine zikisisitiza vipengere hivyo viingizwe na kuwa sehemu ya mkataba.
Aidha nchi zilishindwa kukubaliana pendekezo lililokuwa limetolewa na mataifa ya  Kiarabu la kutaka suala la Palestina la kujiamulia mambo yake liingizwe kwenye mkataba. Pendekezo hilo lilipingwa vikali na nchi za Ulaya na Marekani.
Vipengele vingine ambavyo vimechangia kutopatikana kwa Mkataba huo, ni kuhusu pendekezo la kutaka Taasisi na Mashirika ya Kikanda yanayo jihusisha na kuangalia matumizi ya silaha kutaka yapewe nafasi katika Mkataba  huku baadhi ya nchi zikipinga pendekezo hilo.
 Halikadharika, suala la Haki za kijinsia  lilichagizwa na baadhi ya nchi likitaka liingizwe kwa kisingizo kwamba matumizi holela ya silaha yamekuwa ya kisababisha matatizo makubwa. Baadhi ya nchi  hususani za Afrika zilipinga kuingizwa kwa kipengele hicho  zikitumia kigezo  kwamba hadi sasa hakujawa na tafsiri sahihi ya neno  usawa wa kijinsia kutoka na baadhi ya mataifa ya magharibi kulazimisha kutambua haki za mashoga.
Kipengere kingine kilihusu  kuingizwa kwa risasi kwenye  mkataba,  jambo lilozua  mvutano na  mabishano makali, huku nchi kubuwa zikikataa kata kata kuingizwa kwa risasi kwenye  mkataba  huku zikitishia kwamba zisingekuwa tayari kusaini mkataba huo kama risasi zingeingizwa.wapo

“Ninasikitika sana kwamba tumefika hapa tulipofika, hayakuwa matarajio yangu mimi kama rais wa mkutano huu na wala hayakuiwa  matarajio yenu. Yalikuwa ni majadiliano magumu,  yaliyojaa hisia kali tulijitahidi tulivyoweza kujaribu kuweka sawa maslahi ya kila upande.  Lakini tumeshindwa kutoka na  Mkataba” akatamka Balozi Roberto Garcia  Morita wa Argentina aliyekuwa Rais wa Mkutano huo.
Akiongea kwa  masikitoka  makubwa   Balozi  Roberto Morita amesema kukata tamaa. “ Sitaki kusema mengi nisije nikatafsiriwa vibaya, ninaomba nibebe dhamana hii ya kushindwa kufikia malengo ya kuwa na mkataba. Nawashukuruni nyote kwa hatua hii tuliyofikia ingawa tumeshindwa kukidhi hamu na matarajio ya watu”.
Ingawa majadiliano kuhusu kuanzishwa kwa mkataba wa kudhibiti biashara  ya silaha yalikuwa magumu na ingawa mkataba huo haukupatikana. Lakini majadiliano hayo yaliwezesha kupatikana kwa Rasimu ambayo kama isingekuwa kwa vipengele vilivyotajwa hapo juu kuzua mvutano katika siku za mwisho basi Mkataba ungepatikana. hatimaye chini ya usimamizi wa raisi wa mkutano huo.
Karibu nchi zote ambazo zilipata nafasi ya kuzungumza baada ya Rais kutamka kuhitimisha kwa mkutano huo, ziliongea kwa hisia na kuelezea namna gani  zilivyosikitishwa na matokeo hasi ya mkutano huo. Lakini zikaahidi kwamba zitakuwa tayari kuendelea na majadiliano hapo baadaye na hasa kwa vile sasa wanatambuana vilivyo na wanajua misimamo ya kila nchi.
Baadhi ya nchi kama vile Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, mjumbe wake aliezea kwamba kushindwa kupatikana  kwa mkataba huo ni kielelezo cha wazi kwamba wananchi wa DRC ambao hawajawaji kuonja amani na usalama kwa miaka mingi wataendelea kuathirika.
“ Sote tunajua kwa nini tumefika hapa, silaha ni biashara ya pili kwa ukubwa baada ya ile ya madawa. Ni kweli  tunasikitika kwa matokeo haya lakini hatujakata tamaa, tutaendelea kujadiliana ili hatimaye tuje kuwa na mkataba wa kudhibiti silaha. katika siku za baadaye tuje kuwa na mkataba.
Mkataba huo wa Kisheria kwa Kudhibiti Biashara ya Silaha Duniani kama ungepatikana  basi  silaha ambazo zingeguswa na  mkataba  ni pamoja na Magari ya Deraya, Helkopta za kivita, ndege za kivita, vifaru, magari ya kubeba  mizinga, makombora,   silaha ndogo na  nyepesi
Aidha mkataba huo pia ungedhibiti suala zima la ununuzi wa silaha hizo,  usambazaji ,matumizi  yake  na kuhakikisha kwamba haziangukii mikononi mwa wahalifu.

0 comments:

Post a Comment

Mdau mtandao huu ni kwa ajili yako, weka maoni yao uelimishane na wenzako, Zingatia kutoleta maoni yanayochafua hali ya Hewa! Sasa Endelea....