Wednesday, July 4, 2012

PALESTINA INAPOAMUA KUWA NGANGARI YAKWAMISHA KUANZA KWA MKUTANO KUHUSU MKATABA WA BIASHARA YA SILAHA

0 comments
NA MWANDISHI MAALUM, NEW YORK
Licha ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,   Ban Ki Moon kuufungua rasmi mkutano wa nchi wajumbe wa majadiliano kuhusu  kuanzishwa  kwa mkataba wa  Kimataifa wa Biashara ya Silaha Duniani ( ATT). Majadiliano rasmi ya mkataba huo  yalikwama kuanza  kwa siku mbili baada ya  kutolewa hoja ya kutaka Palestina ishiriki katika mkutano huo kama nchi na si muangalizi ( Observa).
Hoja hiyo ambayo iliamusha malumbano na mabishamo kati ya Palestina na nchi za Magharibi iliwasilishwa siku ya jumatatu na  nchi ya Misri.
Mkutano  huo  muhimu sana kwa  mustakabari wa  biashara ya silaha na kwa usalama wa  maisha ya  watu, ulitakiwa kuanza rasmi siku ya jumatatu  lakini hali haikuwa hivyo baada ya  Misri kuwasilisha hoja hiyo.
Baada ya kushindikana kuanza siku ya jumatatu, mkutano uliahirishwa hadi siku ya jummane, hata hivyo mkutano ukashindwa kuanza kwa muda uliopangwa  kutokana na kutofikiwa  kwa muafaka wa hoja ya kutaka  Palestina ishiriki kama nchi kamili.
Hatimaye mkutano ulianza kwa Ban Ki Moon kutoa hotuba yake ambayo aliwasihi wajumbe wa mkutano huo kumaliza tofauti zao kidiplomasia ili  mkutano huo muhimu  uweze   kuanza.
 Hata hviyo baada ya   Ban Ki Moon kutoa hotuba yake na kuondoka,  hali iliendelea kuwa ya sintofahamu kutokana na pande zinazohusika kuendelea kuvutana na kutofikia muafaka wowote.
Taratibu na sheria za mkutano huu wa kimataifa  unaojadili maadalizi ya mkataba wa kudhibiti biashara ya silaha zinaeeleza kwamba washiriki wa mkutano  huo ni  nchi za jumuia ya kimataifa  bila ya kujali kwamba nchi  hiyo ni Mwanachama kamili wa Umoja wa Mataifa.
Palestina inajulikana kama  nchi mtizamaji   kutokana na kwamba bado haijatambuliwa au kukubaliwa kama mwanachama wa Umoja wa Mataifa.
  Na kwa sababu hiyo imekuwa ikishirika mikutano ya Umoja wa Mataifa kama nchi mwangalizi na kwa taratibu za umoja wa mataifa nchi mwangalizi haipewi haki stahili za kujadili, kuchangia au kutoa maoni   kama  ilivyo kwa nchi ambayo ni mwanachama. Na kama ikipata  fursa ya kuzungumza basi huzungumza mwisho  kabisa  baada ya nchi wanachama kuzungumza.
 Mvutano huo wa aina yake, ambao hatimaye suluhu  ilipatikana kwa waandaaji wa mkutano huo kukubali  kuipatia Palestina  hadhi ya kushiriki mkutano huo kama mwanachama. Na kuepusha uwezekano wa kuipigia kura hoja hiyo
 Kufuatia kumalizika mwa mvutano huo, majadiliano rasmi yalianza siku ya jumanne saa moja usiku.
Hata hivyo uamuzi wa kuiruhusu Palestina kushirikia kwa asilimia mia  majadiliano ya mkutano huo, kulizua   manung’uniko kutoka nchi ya Holy Sea ( Vatican) ambayo kupitia mjumbe wake ilisema haikutendewa haki kwa sababu kwa mujibu wa kanuni za mkutano huo ilipashwa nayo kushiriki mkutano  ikiwa na haki zote kama nchi mwanachama.
Mjumbe wa Holy Sea alieleza kinagaubaga na huku akinukuu maazimio mbalimbali kwamba sekretarieti ilikuwa inaweka  historia  mbaya huku ikikiuka maazimio ya  Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Holy See ikasema mkutano  huu unaojadili maandalizi ya mkataba wa biashara ya silaha, ni mkutano muhimu na nyeti unaogusa maslahi ya kila nchi. Na  ni mkataba ambao ukishaandaliwa na kupitishwa utazigusa nchi zote.
Na kwa sababu hiyo akasema mjumbe huyo wa Holy Sea, kwamba ni kutokana na ukweli huo, na  kwa kuzingatia kwamba Holy Sea imekuwa ikifuatilia kwa karibu mchakato mzima wa majadiliano ya  kuanzishwa kwa mkataba huo, Hivyo basi  ilikuwa inastahili kushiriki kwa asilimia mia moja. Na kusisitiza kwamba hoja yake iingizwe  kama hoja rasmi katika kumbukumbu za mkutano huo.
Awali akifungua mkutano huo, Ban Ki Moon amesema kwamba ma- milioni  ya watu wanapoteza maisha kila mwaka kutokana na matumizi yasio sahihi ya silaha.
Aidha akabainish kuwa  dola za kimarekani Trillion moja hutumika kila mwaka kwaaajili  kujilimbikiza silaha za kijeshi.
Kama hiyo haitoshi Ban Ki Moon anasema  utafiti uliofanywa kwa  nchi za Afrika kati ya mwaka 1990 hadi 2005, nchi  23 za Afrika zilipoteza kiasi  dola za kimarekani bilioni 284 kutokana na  migogoro ya kivita.
“ Matumizi mabaya na kuto ratibiwa kwa biashara ya  silana,  kumeongeza mateso kwa raia wasio na hatia ambao wanajikuta kati  kati ya mapambano. Tunayaona haya katika  mauaji  yakiwamo madhara wayapatayo watoto” akasema  katibu Mkuu na kuongeza.
Dunia inatuangalia, watu wanatuangalia, wanataka siye tuliokusanyika  katika ukumbi huu tuwape matumaini, tuwape matumaini kwamba mwishoni mwa mkutano huu tutatoka na mkataba wa kimataifa kwa kudhibiti biashara ya silaha.
“ Hebu tuutazame ukweli, jukumu lilopo mbele yetu ni kubwa na zito na kuna changamoto kubwa kufikia  kile tunachokita. Biashara ya silaha inagusa maslahi ya nchi nyingi”. Akabainisha Ban Ki Moon
“ Nimefurahi sana kwamba ukumbi huu umejaa kupita kiasi, na hili linadhihirisha ni kwa namna gani tunalipa uzito suala hili, tunajukumu nzito, lazima tufike mahali tukubaliane kuto kukubaliana, tuweke kando tofauti zetu, mwisho wa mkutano tutoke na mkataba, mkataba  utakaowapa watu matumaini” akasihi Ban Ki Moon.
Hata hiyo duru za kidiplomasia zinatahadharisha kwamba kuna uwezekano mkubwa kwamba mkutano huu ambao ni wa mwezi mmoja unaweza usitoke na jambo lolote la maana achilia mbali mkataba.
Na hii inatokana na misimamo mbalimbali ya kimaslahi inayooneshwa na mataifa achilia mbali yale yaliyoendelea bali hata yale yanayoendelea na kubwa sana ikiwa ni  kulinda maslahi yatokanayo na biashara hiyo.Mchakato wa majadiliano kuhusu kuanzishwa kwa mkataba wa biashara ya  silaha duniani yalianza miaka  sita iliyopita baada ya  Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupitisha azimio lilokuwa likiagiza pamoja na mambo mengine kuanzishwa kwa majadiliano ya kuwapo kwa mkataba huo. 

.....Sasa wakisema tunapiga kura   hapa pame kaa vipi, ndivyo anavyoonekana kusema,  Brigedia General Charles Muzanizanila kutoka  Jeshi la Wananchi wa Tanzania ( JWTZ ) akiwa katika  majadiliano na Kaimu Balozi wa  Ubalozi wa  Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Justin Seruhere. Dkt. Seruhere na Brigedia  General Muzanizanila wanaongoza  ujumbe wa Tanzania katika  mkutano wa mwezi mmoja wa   nchi Wajumbe wa majadiliano kuhusu Mkataba wa  Biashara ya Silaha ( ATT). viongozi hawa wawili   kama ilivyokuwa kwa wajumbe wengine, walijikuta wakitafakari hatima ya maendeleo ya mkutano huu, baada ya kutokea mkwamo uliosababishwa na nchi ya Misri kuamua kuwasilisha hoja siku ya kwanza  ya kuanza kwa mktano huo ( jumatatu) hoja ya kutaka  Ujumbe wa Palestina uruhusiwe kushirika mkutano huo kama nchi kamili na si mtizamaji (observa)

0 comments:

Post a Comment

Mdau mtandao huu ni kwa ajili yako, weka maoni yao uelimishane na wenzako, Zingatia kutoleta maoni yanayochafua hali ya Hewa! Sasa Endelea....