Tuesday, July 3, 2012

WAZIRI KABAKA ALONGA UMOJA WA MATAIFA

0 comments
NA MWANDISHI MAALUM, NEW YORK
Wakati Jumuia ya kimataifa ikiendelea kukuna vichwa kutafuta mbinu na mikakati ya  kukabiliana na  hatari inayotokana  na  ongekezo kubwa la ukosefu wa ajira  na hususani kwa Vijana. Tanzania  inasema kwa kutambua ukubwa wa tatizo hilo imeanza kuandaa mikakati endelevu ya kulikabili janga hilo.
Akizungunza katika siku ya pili ya  mkutano  unaowakutanisha kwa pamoja mawaziri wanaohusika na masuala ya ajira, wataalamu wa masuala ya fedha , uchumi na  wanazuoni. Waziri wa   Kazi na Ajira, Mhe. Gaudentia Mugosi Kabaka ( Mb) anasema Tanzania  kama ilivyo kwa nchi  nyingine zinazoendelea inakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa ajira.
Mhe. Waziri Kabaka anaongoza  ujumbe wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mkutano wa wiki moja unaofanyika hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa. Mkutano huo ambao umefunguliwa na  Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki  Moon mwanzoni mwa wiki,   umeandaliwa na  Baraza la Umoja wa Mataifa linalohusika na  masuala ya  Uchumi na Maendeleo ya Jamii (ECOSOC).
“Kama ilivyo kwa nchi nyingine  zinazo endelea duniani, nchi yangu pia inakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa ajira  na hasa kwa vijana. Na  tatizo hili linasababishwa kwa kiasi kubwa na uboreshaji wa elimu yetu  hadi ngazi ya elimu ya juu, uboreshani na upanuzi ambazo hauendani sambamba na  ongezeko la ajira”.
Amewaeleza wajumbe wamkutano huo kwamba, tatizo la ajira pia  lipo zaidi kwa upande wa mijini na hii ni kutoka na wimbi la vijana kuhamia mijini.
“ licha ya kwamba vijana wengi wanahamia  mijini na hivyo kuchangia katika ukosefu wa ajira, lakini pia hivi sasa tunashuhudia vijana wale wa vijijini kukoa ajira kutokana na athali za mabadiliko ya tabia nchi , mabadiliko ambayo  yamekuwa na athari kubwa kwa upande wa kilimo” akabainisha  Kabaka.
Akaitaja baadhi ya mikakati inayofanywa na serikali ya kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana, kuwa  ni pamoja na  mpango wa kurasimisha  mali za wanyonge ( Mkurabita) ili mali hizo ziweze kutumika kupata mikopo, upanuzi vya  vyuo vya ufundi stadi ili vijana waweze kujiajiri wenyewe, na  kuanzishwa pamona na mambo mengine  sheria ya   hifadhi ya jamii, mifuko ya  jamii, mifuko ya bima ya afya,  na vyama vya   ushirika vya kuweka na  kukopa ( SACCOS)
Aidha akasema, serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali  ziwamo taasisi za  kitaifa na kimataifa, imekuwa ikiratibu mafunzo mbalimbali yakiwamo ya uwezeshaji katika eneo la kilimo ili vijana wawe kujiajiri katika eneo hilo na kwamba mipango yote inalenga katika kufanikisha utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya millennia.
Aidha akasema, Tanzania pia inaendelea na jukumu la kuhakikisha kwamba  ajira kwa watoto inakomeshwa, kuwapo kwa ajira zenye tija, endelevu na zenye hadhi na kwa sababu hiyo akauomba Umoja wa Mataifa kupitia  ECOSOC, kuisaidia Tanzania  katika eneo la  teknolojia.
Mada kuu ya mkutano huu  ni kukuza uwezo wa uzalishaji wa ajira kwa vijana, na kazi zenye heshima kwa lengo la kuondokana na umaskini na kukuza uchumi endelevu ili kufikira utekelezaji wa MDGs.
Mkutano huo unatoa  fursa kwa nchi wanachama wa UMum kujadiliana na kubadilishana mawazo kuhusu masuala ambayo ni changamoto kubwa kwa usalama wa dunia. Na  hususani wimbi hilo la ukosefu wa ajira kwa vijana,  wimbi ambalo limesha onesha kwamba lisipotafutiwa mikakati ya kudumu ni bomu ambalo tayari limeshaanza kufuka moshi.

0 comments:

Post a Comment

Mdau mtandao huu ni kwa ajili yako, weka maoni yao uelimishane na wenzako, Zingatia kutoleta maoni yanayochafua hali ya Hewa! Sasa Endelea....