Thursday, August 2, 2012

SIMBA KUMTANGAZA NGASSA KESHO

0 comments
Ngassa
DAR ES SALAAM, TANZANIA
KLABU ya Simba kesho inatangaza kumtwaa rasmi mchezaji nyota, Mrisho Ngasa, baada ya kufanikiwa kuipiku Yanga, kwa kumpata mchezaji huyo kwa mkopo
  "Klab ya soka ya Simba inawakaribisha kwa dhati kesho kuhudhuria mkutano wake na waandishi wa habari utakaofanyika katika Ukumbi wa Makao Makuu ya Klabu Mtaa wa Msimbazi Saa TANO KAMILI ASUBUHI....NYOTE MNAKARIBISHWA. Ni mkutano utakaokuwa na habari nzito. Msikose" Amesema Ofisa habari wa Simba Ezekiel Kamwaga.

Timu ya Azam imeamua kumtoa kwa mkopo kwenda Simba mchezaji nyota hapa nchini, Mrisho Ngassa, huku Yanga ikitakiwa kujikamua dola za Marekani 50,000 ambazo ni takribani sh. milioni 80 za Tanzania, ili iweze kumrejesha kundini kwake mchezaji huyo ambaye anaaminika kuwa ni kipenzi cha Yanga.

 Taarifa iliyotolewa na Meneja wa klabu ya Azam Patrick Kahemele, imesema kuwa biashara ya Azam kumuuza Ngassa imefanyika kwa uwazi.

" Azam FC ilitangaza kuwa biashara ya mchezaji Mrisho Ngasa ingefungwa siku ya Jumatano 1/08/2012 saa saba mchana na ilivitaka vilabu vyenye kumhitaji mchezaji huyo kufika makao makuu ya Azam FC zikiwa na pesa taslimu. bei ya mauzo iliyopangwa ilikuwa ni dola 50,000 xa Marekanini katika mawasiliano ya email kwa makatibu wakuu wa Simba na Yanga, Azam FC iliweka bayana kuwa ilikuwa tayari kushusha bei ya mauzo na ingemuuza Ngasa kwa timu ambayo dau lake lingekuwa kubwa zaidi ya mwenzake", imesema taarifa ya Meneja wa klabu ya Azam Patrick Kahemele.

Ameongeza katika taarifa hiyo kwamba biashara ya mchezaji Ngasa ilifanyika kwa uwazi na kwamba lengo la Azam FC lilikuwa ni kutoa haki kwa kila klabu yenye uwezo wa kifedha kuweza kupata huduma ya Ngasa.

"Pia tunaomba ifahamike bayana kuwa mchezaji Mrisho Ngasa alipewa taarifa kuwa anauzwa na aliombwa asaidie kushawishi klabu anayoitaka ifike kwetu na ofa yake. Ngasa alitamka bayana kuwa yupo tayari kwenda klabu yoyote ambayo Azam FC itaona imekidhi mahitaji yake kwa masharti kuwa maslahi yake ya kimkataba kati yake na Azam FC yazingatiwe", alisema meneja wa Azam.

Amesema hadi Jumatano, 01/08/2012 saa saba mchana ni Simba pekee iliyojibu kwa maandishi na kuonesha nia ya kumchukua Ngasa lakini Yanga wao hawakuwahi kujibu email, ingawa kwa majibu ya simu Mjumbe wao wa Kamati ya usajili Bw Sefu Magari alitangaza kuwa Ngasa hana thamani ya zaidi ya milioni 20 na Yanga haikuwa tayari kuboresha ofa yake.

Kwa mujibu wa meneja huyo wa Azam, muda wa kufungwa kwa biashara ya kumuuza Ngasa ulipofika, ni simba pekee kupitia kwa makamu Mwenyekiti wake Bw Geofrey Ngange na Mhasibu wake ndiyo waliofika wakiwa na pesa taslimu shilingi milioni 25 huku Yanga wakiwa hawakuonekana na hawakutaka kupokea hata simu walizokuwa wakipigiwa kuulizwa kama wana interest.

Kikao cha dharura cha Azam FC kilikaa na kuamua kuwa biashara ya kumuuza Ngasa ilishindikana kutokana na kutokupatikana kwa mnunuzi mwenye dola 50,000. Kwa maana hiyo Azam FC iliamua kumpeleka Ngasa kwa mkopo kwenye klabu iliyofika na kuonesha nia ya kumhitaji mchezaji huyo.

Simba wamepewa sharti la kuhakikisha wanamlipa Ngasa mshahara wake kamili (TZsh 2,000,000) pamoja na stahiki zake nyingine zote za kimkataba

Meneja huyo amese,a  sababu za kumpeleka Ngasa kwa mkopo ni kumuepusha na adhabu ambayo klabu ya Azam FC ingetoa kwa Ngasa kama angebaki.

"Azam FC inapenda kuweka wazi kuwa haijamlazimisha Ngasa kwenda Simba kama inavyopotoshwa. Kama Ngasa anataka kuvunja mkataba wake au kama Yanga bado wanamhitaji basi waje na dola 50,000 na Azam FC itawauzia kwani licha ya kwamba amepelekwa kwa mkopo simba lakini Ngasa bado ni mali ya Azam FC" Alisema meneja wa Azam na kuongeza:

 "Tunaomba kuweka msimamo wetu kuwa hatupo tayari kumlipa Ngasa na kuvunja mkataba wake na hatuna sababu ya kufanya hivyo. Kama Ngasa hataki kwenda tunakompeleka Azam FC inamruhusu kubakia klabuni na kutumikia adhabu".

Adhabu inayomnyemelea Ngassa kama atabaki Azam ni kwamba, akibaki timu hiyo atakaa nje ya uwanja kwa muda wote uliosalia kwenye mkataba wake kutumikia adhabu ya kosa la kufanya vitendo vya utovu wa nidhamu anavyodaiwa kufanya.

0 comments:

Post a Comment

Mdau mtandao huu ni kwa ajili yako, weka maoni yao uelimishane na wenzako, Zingatia kutoleta maoni yanayochafua hali ya Hewa! Sasa Endelea....