Saturday, September 1, 2012

RAIS KIKWETE AKUTANA NA KAIMU WAZIRI MKUU WA ETHIOPIA

0 comments

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete  Jumamosi, Septemba Mosi, 2012 amekutana na kufanya mazungumzo na Kaimu Waziri Mkuu wa Ethiopia Mheshimiwa Hailemariam Desalegn.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika kwenye Hoteli ya Sheraton mjini Addis Ababa ambako Rais Kikwete amefikia wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku tatu yalichukua kiasi cha nusu saa.

Katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete amerudia salamu zake za rambirambi ambazo amekuwa anazitoa kwa wananchi wa Ethiopia na uongozi wake tokea kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, mheshimiwa Meles Zenawi.

“Nataka tena kuwasilisha rasmi salamu zangu za rambirambi na za wananchi wa Tanzania kwako wewe kwa niaba ya wananchi wa Ethiopia kufuatia kifo cha Mheshimiwa Meles. Hakuna shaka kuwa siyo Ethiopia tu
iliyopoteza kiongozi shupavu bali Afrika nzima imepoteza kiongozi hodari sana. Sisi katika Tanzania tumekuja kuungana nanyi katika msiba huu mkubwa. Napenda tu kukuhakikishia kuwa machungu yenu ni machungu
yetu,” Rais Kikwete amemwambia Mheshimiwa Desalegn.

Ameongeza Rais Kikwete: “Nilikuwa na uhusiano mzuri na wa karibu wa kikazi na Mheshimiwa Meles. Napenda kukuhakikishia kuwa nitaendeleza uhusiano huo nawe. Najua kuwa huu ni wakati mgumu kwa Ethiopia kwa sababu nchi hii haina uzoefu wowote wa jambo kama hili la kufiwa na kiongozi. Naelewa ilivyo vigumu kwetu lakini nina hakika kuwa mnao uwezo na uvumilivu wa kutosha wa kukabiliana nalo.”

Naye Mheshimiwa Degalegn amemshukuru Rais Kikwete kwa uamuzi wake wa kuja Ethiopia kushiriki katika mazishi ya Mheshimiwa Meles. “Najua kuwa umekuja kwa ajili ya msiba lakini nataka kukuambia kuwa sisi
katika Ethiopia tunaiona siku hii kama siku muhimu sana kwa kuweza kupokea kiongozi muhimu sana wa Tanzania.”

Ameongeza Mheshimiwa Degalegn: “Ni dhamira yetu kubwa kuhakikisha kuwa uhusiano mzuri kati ya Ethiopia na Tanzania ambao Mheshimiwa Meles aliuendeleza kwa bidii sana utaimarishwa zaidi hata baada ya yeye kuwa ameondoka duniani.”

Rais Kikwete amewasili Ethiopia mapema leo kwa ziara ya kikazi ya siku tatu ambako miongoni mwa mambo mengine atashiriki mazishi ya Mheshimiwa Meles kesho.

0 comments:

Post a Comment

Mdau mtandao huu ni kwa ajili yako, weka maoni yao uelimishane na wenzako, Zingatia kutoleta maoni yanayochafua hali ya Hewa! Sasa Endelea....