Tuesday, October 16, 2012

MANONGI:TUACHE MALUMBANO TUJADILI HALI HALISI

0 comments

                                                                     NEW YORK, MAREKANI
Wakati   Baraza la  Uchumi na Fedha  ( ECOSOC) la  Baraza  Kuu la Umoja wa  Mataifa, likizindua Tathmini ya Miaka Minne ya Shughuli za Maendeleo ya Umoja wa Mataifa  ( QCPR). Tanzania imetaka  majadiliano ya tathimini hiyo yalenge zaidi katika kujadili hali halisi ya mambo badala ya nchi kujitafutia umaarufu.
Akichangia majadiliano hayo Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi amesema, tathimini hiyo inafanyika katika kipindi ambacho mdororo wa uchumi ukiendelea kuitikisa dunia na kiwango  cha umaskini kikiongezeka.
“  Mengi yamekwisha kuzungumzwa na wasemaji walionitangulia kuhusu tathmini hii. QCPR inajadiliwa  wakati mtikisiko wa uchumi ukiendelea duniani na umaskini ukiongezeka. Na pia tunashuhudia  kushuka kwa kiwango cha misaada ya maendeleo inayotolewa  kwa nchi zinazoendelea. Hebu basi na tutumie majadiliano haya kujadili  ukweli halisi wa  mambo yalivyo badala ya kujadiliana nafasi ya nchi au umaarufu wa nchi”.Akasisitiza Balozi Manongi.
  Tathimini hiyo ya miaka minne ambayo inalenga katika kupitia utekelezaji wa  mipango ya   maendeleo zikiwamo será mbalimbali  itahusisha  Mashirika, Taasisi na Mifuko iliyochini ya Umoja wa  Mataifa na ambayo kwayo imekuwa ikitumika kufadhili miradi na programu mbalimbali za Maendeleo.
 Mashirika  na Taaisisi hizo  11  ikiwamo miradi ya utafiti na  mafunzo ni pamoja UNDP, UNICEF, WFP. UNHCR. UNCTAD na UNEP.
Balozi Manongi amesema Tanzania  inapenda kusisitiza umuhimu wa  mipango   ya  Umoja wa Mataifa katika ngazi ya nchi,  mipango ambayo  hususani ile ambayo  imeainishwa na nchi  zenyewe.
“ Mipango hii yote inalenga katika kutusaidia sisi katika kukabiliana na changamotoz zetu.  Mwezi  June mwaka  jana, Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na  Umoja wa Mataifa ilizindua Mpango wa Misaada ya Maendeleo  ( UNDAP). Mpango huu unaelezea ushirikiano wetu na Mashirika 20 ya UM ikiwamo Mifuko na   Programu katika maeneo ya ukuaji wa uchumi na upunguzaji wa  umaskini,  uboreshaji wa maisha, ustawi wa jamii, utawala bora, masuala ya dharua na udhibiti wa maafa na uhifadhi wa wakimbizi” akabainisha
Na kuongeza kwamba Ujumbe wa Tanzania katika  mkutano huo umefarijika sana kwamba  QCPR inafanyika sanjari na kilele cha mpango wa  majaribio wa  Ufanyaji kazi wa Pamoja wa Umoja wa Mataifa (  Delivering as One).
“ Ni matumaini yetu kwamba  matokeo ya utafiti wa tathmini  huru ya  DaO itaendelea  kutujulisha  kuhusu mchakato wa mapitio. Jambo moja ni wazi kwamba nchi ambazo zimejitolea kutekeleza mpango huu zingependa kuudumisha na kuendelea nao”. Akasisitiza Balozi
Na kuongeza kwamba tangu kuanza kwa majaribio  mwaka 2007 nchi nyingi zimeukubali na litakuwa jambo la kusikitisha kama QCPR haitautilia maanani.
Aidha kama ilivyokuwa kwa wasemaji wengine, Tanzania pia ilirejea wito wake wa kutaka kuimarishwa kwa Ofisi ya Mratibu Mkazi  ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa ukamilifu. Huku ikisisitiza kwamba mafanikio ya utekelezaji wa DaO ishuke hadi katika  ndani ya Umoja wa Mataifa.
Aidha  Tanzania pamoja na mambo mengine imesisitiza haja na umuhimu wa uboreshaji wa njia za utekelezaji wa DaO. Na kwamba anatoa wito wa Bodi zote zinazosimamia Mashirika, Mfuko na Programu kupitia mifumo yao ya utendaji  kwa lengo la kuimarisha uratibu na ushirikiano ili kupunguza gharama. 
Awali akizindua Tathimini hiyo, Naibu  Katibu Mkuu wa UM,Bw. Jan Eliason alitoa changamoto kwa  Umoja huo kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia hali halisi ilivyo hivi sasa. 
Akasema “ mazingira ya  changamoto za maendeleo   yamebadilika,  mataifa mengi yanazidi kutambua kuwa  chombo hiki  kinahitaji kutekeleza wajibu wake vizuri zaidi kwa kushughulikia  matatizo mtambuka ya kiuchumi, kijamii  na kimazingira” akasema na kuongeza “  ni miaka michache tu  iliyopita ambapo zaidi ya nusu ya nchi ambazo hivi sasa zinatambuliwa kama nchi zenye uchumi wa kati, zilikuwa ni nchi ambazo uchumi wake ulikuwa mdogo”.
  Na kwa sababu hiyo anasema kwamba wakati UM ukizindua tathimini hiyo ya maiaka minne ya shughuli zake za maendeleo, lazima itambue kwammba maendeleo endelevu ndiyo nguzo na kiini katika kipindi hiki ambacho idadi ya  wadau wa ushirikiano wa maendeleo wakiongezeka.
“ Hivi sasa ushirikiano wa kimaendeleo siyo tena uwanja unaohodhiwa na  nchi Fulani au mashirika ya kimataifa” akasema  na kusisitiza “ hivi sasa tunategemea zaidi michango ya sekta binafasi,  mifuko ya kijamii,  wanazuoni na  vyama   vya kijamii. Mfumo wa Umoja wa Mataifa unatakiwa kuanza kubuni njjia mbadala na sahihi za kuunganisha nguvu za wadau hawa wapya”.                                                     

0 comments:

Post a Comment

Mdau mtandao huu ni kwa ajili yako, weka maoni yao uelimishane na wenzako, Zingatia kutoleta maoni yanayochafua hali ya Hewa! Sasa Endelea....