Friday, October 19, 2012

TANZANIA YAISHAURI ICC KUJIEPUSHA NA USHAWISHI WA KISIASA

0 comments

NA MWANDISHI MAALUM, NEW YORK, MAREKANI
TANZANIA imeishauri Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai ( ICC) kutekeleza majukumu yake  bila ya ushawishi wa kisiasa  kutoka nchi yoyote  likiwamo Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Ushauri huo umetolewa na Balozi wa  Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Matiafa, Tuvako  Manongi (pichani), wakati  wa mjadala wa wazi uliohusu   uhusiano kati ya   Amani na Haki na  Mahakama ya  Kimataifa ya  Makosa ya Jinai ( ICC). Mjadala huo uliandaliwa na    Baraza Kuu la Usalama la  Umoja wa Mataifa.

Akizunguma katika  mjadala huo uliofunguliwa na katibu Mkuu wa UM, Ban Ki Moon, Balozi Manongi amesema, ili   Mahakama hiyo   iweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo inapashwa kujiepusha na ushawishi  au mashikinikizo ya kisiasa.

Akafafanua kwamba, kwa Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine ambazo zimekwisha kuitambua mahakama hiyo, inategemea na inaamini kwamba  itatekeleza majukumu yake bila ya upendeleo wa aina  yoyote ile.

Akaeleza wazi kwamba nchi nyingi  hasa zile za Afrika zimekuwa zikionyesha  wasi wasi wao juu ya mwenendo wa Mahakama hiyo licha ya ukweli kuwa  , nchini nyingi za  Afrika siyo tu zimeitambua lakini  masuala mengi yanayoshughulikiwa na makahama hiyo  yanaihusu Afrika.

“ Uhuru wa kutoadhibiwa lazima uzingatiwe wakati wowote na mahali popote”. Anasema Balozi na kuongeza. “ Usemi kwa kwamba haki ni lazima itendeke,  lakini vile vile lazima ionekane. Na huu ni ukweli kwa chombo chochote cha kisheria kama inavyotakiwa kufanyika pia katika ICC”. Akasisitiza.

Na kuongeza kwamba ili haki hiyo itendeke na kuonekana ni lazima basi iwe kwa wote bilaya kujali au kuzingatia ushawishi wa kisiasa.

Alifafanua zaidi kwamba   mataifa mengi ya  Afrika yanaona kama vile  uwajibishwaji katika ICC   unalenga upande mmoja.  Na hili ni tatizo  ambalo linapelekea ICC kutopata ushirikiano wa kutosha.

Akaeleza kwamba majukumu ya Baraza Kuu  la Usalama la  UM  na yale ya ICC kwa kiasi fulani yanashabihiana  kutokana na kweli kwamba asilimia kubwa ya majukumu yao yanaihusu Afrika. 

“ Jukumu la kutafuta amani na haki   ni jukumu  la  msingi kwa Baraza kuu na hali kadharika kwa ICC.  Na mara nyingi imeelezwa kuwa   amani haiwezi kuwapo bila haki. Na kwa hakika amani na haki ni kama pande mbili za sarafu zinazotegemeana, kwa sababu  upande mmoja hauwezi kustawi bila ya  mwingine” akasisitiza Balozi  Manongi

Aliongeza, lakini  katika mazingira Fulani Fulani,   Jumuia   ya Kimataifa na Baraza kuu la Usalama zimejikuta zikilazimika kujaribu kutafuta  uwiano  kati ya  pande hizi mbili hasa pale upande mmoja unapoonekana  kuuelemea  upande mwingine.

 “ Ndio maana haishangazi kwamba kitendo cha kutafuta uwiano  kati ya  haki na amani kumezua hofu kubwa. Kutokana na kwamba ni jambo lisiloingia akilini kwa mahakama kutafuta haki kwa gharama ya mchakato wa kutafuta amani. Hata kama itamaanisha kutoa unafuu  wa muda kwa watuhumiwa kutochukuliwa hatua” akasema  Balozi 

Alisisitiza kwamba, mchakato wa kutafuta amani kwa namna yoyote ile usilinganishwe na uhuru wa kutoadhibiwa. 

Aidha  amelitaka Baraza Kuu kuwa wazi zaidi  kwa kutoa maelezo kwa nchi  ambazo zimeomba  uahilishaji  wa mashtaka na hii itasaidia kuboresha ushirikiano na kuondoa hisia potofu dhidi ya ICC.

Halikadharika Mwakilishi huyo wa Tanzania katika UM, anasema   ICC   si chombo pekee  chenye jukumu la kutafuta haki kwa waathirika wa  vitendo vya  jinai. Kwakile alichosema hata nchi  moja moja zinawajibu na haki ya kutafutua haki  kwa waathirika  kwakutumia  taasisi zake  za kisheria, kinachotakiwa ni    kuzijengea uwezo wa kutekeleza jukumu hilo hasa kwa nchi zile ambazo zimetoka katika vita au machafuko.
Kwa upande mwingine, Tanzania  imelitaka  Baraza  Kuu kuisaidia ICC kwa maana ya raslimali ili iweze kutekeleza majukumu yake  ya msingi na vile vile kuzishawishi nchi kutoa ushirikiano kwa mahakama hiyo. 

0 comments:

Post a Comment

Mdau mtandao huu ni kwa ajili yako, weka maoni yao uelimishane na wenzako, Zingatia kutoleta maoni yanayochafua hali ya Hewa! Sasa Endelea....