Sunday, June 16, 2013

IGP AUNDA TIMU KUCHUNGUZA BOMU LILILOUA NA KUJERUHI WATU KWENYE MKUTANO WA CHADEMA, ARUSHA JANA

0 comments
IGP MWEMA
DAR ES SALAAM, Tanzania
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema ameunda timu kwenda kufanya uchunguzi bomu lililolipuliwa mwishoni mwa mkutano wa kufunga kampeni  Chadema, kwenye uwanja wa Soweto  jijini Arusha jana na kusababisha vifo vya watu watatu na wengine 60 kujeruhuhiwa

Akizungumza leo, jijini Dar es Salaam , IGP Mwema amesema timu hiyo itaongozwa na Makamishina wawili kutoka Oparesheni na Idara ya Upelelezi Makao Makuu ambayo itakwenda haraka mkoani kwa ajili ya kuongeza nguvu katika Oparesheni na upelelezi.

Aliwataja watakaongoza timu hiyo kuwa ni Kamishina wa Oparesheni na Mafunzo Paul Changonja na Kamishina Issaya Mngulu, kutoka idara ya Upelelezi wa makosa ya jinai na pia watashirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.

Alisema Jeshi la polisi linalaani sana tukio hilo linaloashiria vitendo vya kigaidi ambalo limesababisha vifo na majeruhi kwa watu wasio na hatia pamoja na kujenga hofu miongoni mwa jamii.

"Napenda kuwahakikishia kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na Oparesheni kali pote nchini kuhakikisha linawasaka na kuwatia mbaroni watu wote waliowezesha, waliofadhili na kutenda uhalifu huo pia nawashukuru wananchi walianza kutupa ushirikiano wa kutupa taarifa za tukio hilo"

Nawashukuru sana wananchi walioanza kutupa taarifa za muonekano, wajihi wa mtu aliyetupa bomu hilo" alisema  Mwema.

Mwema ametoa mwito kwa wananchi kuwa watulivu na kuendelea kutoa ushirikiano wakati uchunguzi ukiendelea na kuwa mtu yeyote mwenye taarifa za wahalifu hao wampigie kupitia namba ya simu yake ya mkoanoni 0754-785557 au katika kituo chochote cha polisi ili kuwakamata wahalifu hao na kuwafikisha mahakamani.

Katika hatua nyingine Mwema ametoa onyo kwamba jeshi la polisi limejipanga kukabiliana na yeyote atakayefanya vitendo vyovyote vya uvunjifu wa amani kwa kutumia fursa ya mchakato wa kupiga kura, kuhesabu kura na kutangazwa kwa matokeo ya chaguzi ndogo zinazoendelea.

Mlipuko huo wa mabomu ni wa pili kutokea mkoani humo katika kipindi kisichozidi miezi mitatu ukifuatiwa na ule uliotokea katika kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi la Oresiti na kuua watu watatu na wengine kujeruhiwa.

0 comments:

Post a Comment

Mdau mtandao huu ni kwa ajili yako, weka maoni yao uelimishane na wenzako, Zingatia kutoleta maoni yanayochafua hali ya Hewa! Sasa Endelea....