Monday, August 19, 2013

CHADEMA WACHAFUA HALI YAA HEWA MWANZA, WAANDAMANA BILA KIBALI, MABOMU YA MACHOZI YARINDIMA

0 comments

MAANDAMANO  yaliyodaiwa kuwa ya  amani yaliyokuwa yameandaliwa na Chadema  jijini Mwanza, yamegeuka shubiri kwa wakazi wa jiji hilo baada ya  polisi kutumia nguvu kutawanya  maandamano hayo.

Maandamano hayo ambayo yalianzia katika eneo la Buzuruga nje kidogo ya jiji la Mwanza yalikuwa yakiongozwa na wabunge Highness Kiwia wa Ilemela  pamoja na Ezekiel Wenje kuelekea katika viwanja vya Furahisha yalilenga kumshinikiza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Ernest Ndikilo kutoa barua zinazodaiwa kuandikwa na ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi kuwarejesha madiwani watatu waliotimuliwa katika Manispaa ya Ilemela kutokana na kushindwa kuhudhuria vikao vitatu mfululizo.

Polisi wenye silaha pamoja na askari kanzu walianza kutanda katika eneo hilo la Furahisha wakiongozwa na Mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai Mkoa wa Mwanza RCO Konyo ambaye alikuwa akitumia gari lenye namba za usajili DK 068EXV aina ya Toyota Land Cruiser

Maandamano hayo ambayo awali yalionekana kama yangelimalizika salama yaliwasili katika viwanja vya Furahisha majira ya saa 5.38 huku yakiongozwa na gari la polisi lenye namba za usajili za nchi ya Uganda  779 UAG likiwa nimesheheni polisi wenye silaha  ikiwa ni pamoja na mabomu ya machozi na bunduki pamoja na askari kadhaa ambao walikuwa katikati ya maandamano hayo.

Baada ya maandamano hayo kuwasili katika viwanja vya Furahisha waandamaji hao ambao walikuwa na mabango mbalimbali yaliyosomeka kuwa ‘Matata hatutaki uendelee kuwa Meya wa Ilemela rudia kazi yako ya awali, na jingine Jaji Sumari tumechoka kuahirisha mara kwa mara kesi dhidi ya Matata na jingine  lililosomeka kuwa RD Ndikilo tunahitaji barua za kurejeshwa kwa madiwani wetu.

Hata hivyo tofauti na ilivyokuwa imetangazwa kuwa maandamano hayo ya amani yangelipokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Ernest Ndikilo, hakukuwa na kiongozi yoyote wa Serikali ambaye alikuwepo uwanjani hapo kupokea maandamano hayo.

Kufuatia kutoonekana kwa kiongozi yoyote wa Serikali,viongozi wa Chadema pamoja na wabunge wao walikutana kwa faragha kwa dakika kadhaa kwa ajili ya kujua hatima ya maandamano hayo ambapo Mbunge wa Nyamagana Ezekiel Wenje alipanda jukwaani saa 6.45 na kuwaeleza maelfu ya waandamanaji kuwa wameamua kumtuma Mbunge wa Ilemela Highnes Kiwia kwenda ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kuchukua majibu kwa ajili ya kuwaletea wananchi walioandamana juu ya hatima ya madiwani hao. Imeandikwa na GSENGO.BLOGSPOT.COM
CHADEMA YATIKISA, NI MABOMU YA MACHOZI KILA KONA YA JIJI LA MWANZA, OFISI, MADUKA  YAFUNGWA.
*****************************************************

0 comments:

Post a Comment

Mdau mtandao huu ni kwa ajili yako, weka maoni yao uelimishane na wenzako, Zingatia kutoleta maoni yanayochafua hali ya Hewa! Sasa Endelea....